Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Boniface Jacob, Jana Jumatano 25/8/2016 alitembelea zaidi ya vikundi 10 vya wajasiriamali ili kuangalia biashara wanazozifanya na kujua changamoto walizonazo.
Meya Jacob katika ziara yake katika Kata za Makumbusho, Sinza, Kawe, Wazo na Kwembe aliongozana na maofisa maendeleo wa Wilaya na Kata pamoja na madiwani ili kusikiliza changamoto za wajasiriamali hao ili waweze kuzitatua.
Wajasiriamali na viongozi wao wa vikundi walimweleza Meya Jacob kwamba changamoto kubwa waliyonayo ni vikundi vingi kuweka akiba lakini waliopatiwa pesa na Dar es Salaam Commercial Bank (DCB) ni wachache na kwamba waliopata haziwatoshi.
Meya Jacob akijibu changamoto hizo, alisema kero hiyo ameipokea katika vikundi vingi hivyo amepanga kuitisha kikao baina ya Manispaa na DCB ili kujua ni kwanini wananchi wanaweka fedha lakini hawapewi hawapati mikopo au awapatiwi mzunguko mwingine wa mkopo kutoka sh 200,000 na sh 350, 000 kufikia sh 700,000 na zaidi.
"Tutawaita na kukaa hao maofisa wa DCB watwambie tatizo ni nini hadi wananchi hawapatiwi mikopo yao....kama wameshindwa kuwahudumia basi waziachie benki zingine kama ya wanawake TWB, CRDB na BENKI ya POSTA kuwahudumia wananchi wa Kinondoni.
Akiwa Kata ya Kawe, ambapo alitembelea katika soko jipya, Meya Jacob, aliwaahidi wajasiriamali hao kufuatilia na kuahakikisha machinjio ya kuku yanajengwa, mitaro na paa la soko hilo linajengwa kwa haraka ili waweze kufanyia biashara maeneo salama na safi.
Katika hatua nyingine, Meya Jacob amempa siku tatu mwenyekiti wa serikali za Mtaa wa Msakuzi Nicolaus Limbugu(CCM) kurejesha fedha za wajasiriamali wa kikundi cha Masawe A. Msakuzi kabla hajachukuliwa hatua za kinidhamu kwa manispaa haikumtuma kuchangisha.
"Natoa wito kwa mwenyekiti huyo kurejesha fedha ya wanakikundi hawa haraka ili ziende benki bar wapatiwe pesa...nitarudi baada ya wiki kujua jambo hili lilipofikia" alisema
Meya Jacob alimtaka ofisa wa Mtaa wa Msakuzi Boaz Maingu kuhakikisha, mwenyekiti huyo Nicolaus anarejesha fedha zote wanakundi 172 na kuweka hesabu yao sawa pasipo malalamiko.
Katika ziara hiyo kwenye Kata tano, aliwashukuru viongozi wa vikundi hivyo kwa kazi yao kubwa ya kuwaweka pamoja, na kuwaahidi kuwaombea posho ndogo ya kuwawezesha kufanya kazi yao vizuri.
Imeandikwa na Janet Josiah.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment